NAIBU WAZIRI WA UJENZI MHE. MHANDISI KASEKENYA AIPONGEZA ERB KWA KUANZISHA SoPE

Wizara ya Ujenzi, kupitia Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), inatarajia kuanzisha Shule ya Wahandisi Wataalamu (SoPE) ili kuboresha ufanisi na umahiri wa wahandisi na wakandarasi nchini. Akizungumzia mpango huu wakati wa kufunga Maonyesho ya MAT Builders Expo, ambayo yalidumu kwa siku kumi katika viwanja vya Mashujaa, Dodoma, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema:
"Kuanzishwa kwa shule hii ni hatua muhimu ya kuongeza ujuzi na taaluma ya wahandisi wetu, hasa katika zama hizi za mabadiliko makubwa ya teknolojia. Wahandisi wanapaswa kujipanga na kuwa na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha miradi ya ujenzi inaleta matokeo bora."
Mhandisi Kasekenya pia alieleza kufurahishwa kwake na mpango huu wakati alipotembelea taasisi mbalimbali za serikali zilizoshiriki maonyesho hayo. Alisisitiza kuwa SoPE itakuwa chachu ya kuwajengea uwezo wahandisi wa kukabiliana na changamoto za teknolojia za kisasa na hivyo kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya ujenzi nchini.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuipongeza Bodi ya Usajili wa Wahandisi kwa juhudi zao za kuimarisha sekta ya ujenzi kupitia mpango huu wa shule ya wataalamu na kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazochangia ukuaji wa teknolojia na ubunifu. Maonyesho haya yaliweka msingi wa ushirikiano na kubainisha njia bora za kukuza ufanisi katika sekta ya ujenzi na uwekezaji wa kisasa nchini.