Msajili wa ERB Apongeza Wahitimu wa Mafunzo ya Ufundishaji wa Taaluma ya Uhandisi ya SoPEL – Morogoro
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Bernard Kavishe, ametoa pongezi kwa wahitimu wa mafunzo ya ukufunzi wa taaluma ya uhandisi yaliyoandaliwa na Shule ya Uhandisi Mahiri na Uongozi (SoPEL), taasisi inayomilikiwa na ERB.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo iliyofanyika mkoani Morogoro, Mhandisi Kavishe alieleza kuwa ERB ina imani kuwa wahitimu hao wataimarisha mbinu za ufundishaji na uenezaji wa maarifa katika taasisi wanazofanyia kazi. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kujifunza mbinu bora za utoaji wa mafunzo ili kuboresha ufanisi wa uwasilishaji.
Mhandisi Kavishe pia alieleza kuwa SoPEL inaendelea kuandaa mafunzo mengine yanayohusu Price Adjustment, yakilenga kuwawezesha wataalamu kufahamu kwa kina eneo hilo ambalo mara nyingi halieleweki vizuri. “Serikali hupoteza mapato si kwa sababu ya wizi, bali kwa kukosekana kwa uelewa sahihi wa masuala ya Price Adjustment. Kupitia mafunzo haya, tunatarajia kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa SoPEL,” alisema.
Kwa upande wake, msimamizi wa shule hiyo, Mhandisi Thereza Laurent, alifafanua kuwa mafunzo hayo yalihusisha zaidi mazoezi ya vitendo ambapo washiriki walipewa nafasi ya kuwasilisha mada wakitumia taaluma na uzoefu wao binafsi katika sekta ya uhandisi.
Miongoni mwa wakufunzi wa mafunzo hayo, Mhandisi Gartius Rwenyagira aliwahimiza wahitimu kushirikisha maarifa waliyojifunza na wataalamu wengine ili kuongeza tija katika taaluma.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Mhandisi Ronald Lwakatare alieleza kuwa mafunzo hayo yamewapa uwezo mkubwa wa kufundisha wenzao kwa kutumia maarifa waliyoyapata. “Tumekuwa tukitegemea wataalamu kutoka nje kuendesha mafunzo, ilhali na sisi tuna uwezo huo. Hatua hii ya ERB ni muhimu kwa maendeleo ya nchi,” aliongeza.
Naye Mhandisi Veronica Ninalwo, Mkuu wa Idara ya Uendelezaji wa Taaluma ERB, alimshukuru Msajili kwa mchango wake mkubwa katika kuanzishwa kwa SoPEL, huku akiwataka wahitimu kuwa mabalozi wa shule hiyo na kuendelea kuhamasisha wataalamu wengine kujiendeleza.
Katika mahafali hayo, wahandisi 14 kutoka taasisi mbalimbali walikabidhiwa vyeti baada ya kuhitimu mafunzo hayo ya siku saba.
19/08/2025
READ MORE