WAHANDISI WATAALAMU 140 WALA KIAPO

Wahandisi Wataalamu 140 wamekula kiapo cha maadili katika hafla ya kongamano na maonesho ya 14 ya Chama cha Wahandisi Tanzania (IET), lililofanyika kuanzia tarehe 04 hadi 06 Disemba 2024 katika ukumbi wa AICC, Arusha. Kiapo hicho kimefanyika leo, tarehe 6 Disemba 2024.
Katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb). Mheshimiwa Majaliwa aliwataka wahandisi waliokula kiapo kuzingatia maadili ya uhandisi katika kazi zao ili kuepuka athari na hatari zinazoweza kujitokeza katika sekta ya ujenzi, akitolea mfano changamoto za kudondoka kwa majengo, jambo ambalo limejitokeza mara kadhaa hivi karibuni.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Lugha Bashungwa, amesisitiza kwamba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi inaendelea kufanya jitihada kubwa kuhakikisha wahandisi wa ndani wanapata fursa zinazolenga kukuza ujuzi na tija, licha ya kwamba kazi nyingi za ukandarasi nchini zinafanywa na kampuni nyingi za nje.
Kiapo hicho ni takwa la Sheria ya Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Sura ya 63, inayowataka wahandisi kufuata maadili na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.