ERB na BAKITA Wajadili Utaratibu wa Tafsiri ya Vyeti vya Taaluma ya Uhandisi kwa Wahandisi Wageni

ERB na BAKITA Wajadili Utaratibu wa Tafsiri ya Vyeti vya Taaluma ya Uhandisi kwa Wahandisi Wageni
Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) imefanya kikao na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) leo, tarehe 7 Machi 2025, katika ofisi za BAKITA zilizopo jijini Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yalilenga kujadili utaratibu wa usajili wa wataalamu wa kigeni wa kada ya uhandisi, hususan kuhusu mchakato wa kutafsiri vyeti vya taaluma ya uhandisi vya wahandisi wageni, ambavyo ni mojawapo ya masharti muhimu katika kupata kibali cha kufanya kazi nchini Tanzania.
Kikao hicho kiliongozwa na Ndugu Shaawal Marinda, Mfasiri kutoka BAKITA, na kilihusisha majadiliano ya kina kuhusu njia bora na sahihi za kutafsiri vyeti vya kitaaluma. Lengo kuu lilikuwa kuhakikisha kwamba tafsiri za vyeti hivyo ni za viwango vya juu, zinaendana na mahitaji ya kitaalamu, na zinaeleweka kwa usahihi na wadau husika.
Aidha, kikao hicho kililenga kutatua changamoto zilizojitokeza katika mchakato wa tafsiri, kama vile utofauti wa istilahi za kiufundi na kiuhandisi katika lugha mbalimbali. Mazungumzo haya yanatarajiwa kuimarisha mchakato wa usajili wa Wahandisi wageni na kuweka msingi thabiti wa ushirikiano kati ya ERB na BAKITA kwa maendeleo ya sekta ya uhandisi nchini.