ERB NA TASAC WAFANYA MAZUNGUMZO

ERB imekutana na Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa mazungumzo yaliyolenga kubadilishana uzoefu katika fani ya uhandisi. Mazungumzo hayo yaliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed M. Salum, akiwa pamoja na wajumbe wake, huku wajumbe wa ERB wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya Ithibati ya Mitaala ya Taaluma ya Kihandisi, Eng. Nerey Mvungi.
Katika mazungumzo hayo, ERB ilipata nafasi ya kujifunza zaidi kuhusu uhandisi wa bahari, ikiwemo changamoto zilizopo, fursa zinazopatikana, na kanuni zinazohusiana na sekta hiyo.
Pia, kikao hicho kiliazimia kuandaa kikao kazi kingine ambacho kitashughulikia uandaaji wa mahitaji (requirements) yatakayowezesha wahandisi bahari kusajiliwa na ERB. Hatua hii inalenga kuwawezesha wahandisi bahari kutambulika kitaaluma na kuthibitisha mchango wao muhimu katika kazi za kihandisi wanazofanya.